0

IMG_0450






Na Eusebius Paul
Hakuna marefu yasiyo na ncha, ndiyo kauli muafaka unayoweza kuitumia ukiisindikiza kwa kushusha pumzi ndefu ili kuruhusu oblongata yako irejee katika utulivu wake wa kawaida.
Hatimaye ligi kuu ya soka nchini Tanzania (bara) inaelekea ukingoni ilhali kila klabu shiriki ikiwa imekwisha tambua hatma yao pindi vipyenga vya mwisho vitakapopulizwa na waamuzi kutoka viwanja vinane tofauti majira ya saa 12 jioni ya Mei 22, Jumapili hii.
Ukiachilia mbali mchuano uliobakia katika kuwania nafasi ya pili ya ligi pamoja na kuepuka kushuka daraja, tayari mabingwa wa msimu wa 2015/16 Dar Yanga Africans wamekwisha kabidhiwa ndoo yao mbele ya maelfu ya mashabiki na viongozi wa kiserikali, lakini hasa mbele ya uwepo wa familia za wachezaji wenyewe. Licha ya figisu nyingi tulizozishuhudia katika msimu huu wa ligi lakini ni dhahiri Yanga waliustahili ufalme huu na kujitwalia tiketi ya kupanda tena ndege kushiriki ligi ya Mabingwa katika msimu ujao, wakati Azam FC wakikata tiketi ya kutuwakilisha tena katika kombe la Shirikisho Africa, pongezi kwao.
Huu ni ubingwa wa 26 kwa Yanga unaoelekea katika viunga vya mitaa ya Kariakoo. Kwa sasahivi suala la ubingwa wa Tanzania kunyakuliwa na vilabu vya Kariakoo siyo habari ya kushtua hata kidogo, iwe Yanga iwe Simba, afadhali uwepo wa Azam FC unaongeza msisimko katika ligi na hata kuutingisha ufalme wa Kariakoo.
Bingwa wa ligi kuu huipeperusha bendera ya Taifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Africa (CCL) wakati bingwa wa kombe la shirikisho hapa nchini huwa na dhamana ya kutuwakilisha katika kombe la Shirikisho Africa (CCC).
Imefikia wakati sasa vilabu vya Tanzania, viongozi, wachezaji na hata wanachama wao kuacha kubweteka na mafanikio ya ubingwa wa nyumbani na kuweka malengo ya kufanya vema zaidi katika michuano ya Africa ambako neema haswa ya mapato hupatikana.
Bingwa wa ligi kuu Tanzania hujipatia kitita cha Tsh. 81 milioni, wakati kombe la shirikisho ambalo fainali yake itapigwa Juni 11 litaambatana na bahasha yenye Tsh. 50 Milioni. Maana yake ikitokea timu yenye ubavu wa kuyabeba makombe yote mawili itajihakikishia Tsh. 131 milioni ndani ya msimu mmoja. Hii ni baada ya kucheza mitanange zaidi ya 35 katika makombe yote mawili, lakini michongo ya maana zaidi hupatikana kwenye michuano ya kimataifa. Mpango kamili uko hivi yaani….
Fedha Zinazovunwa Katika Michuano Ya Africa
Michuano ya ligi ya Mabingwa Africa (CCL) ambayo huwakutanisha wakali kutoka mataifa 54 huambatana na zawadi ya Tshs. 3,282,000,000 (Billion 3.2), timu inayokamata nafasi ya pili hujikamatia Tsh. 2.8 billion, ilhali kutia tu mguu nusu fainali kunawaingizia Tsh. 1.5 billion, achilia mbali kufuzu hatua ya nane bora ambako ni uhakika wa Tsh. 875 million mpaka 1 billioni kulingana na nafasi utakayomaliza ndani ya kundi.
Upande wa Kombe la Shirikisho barani Africa (CCC) nako si haba, bingwa hupata 1.3 billioni na mshindi wa pili akipata 950 million. Wakati timu zinazofaulu kuingia Robo fainali (hatua wanayoipigania Yanga kwa sasa) zina uhakika wa kushinda Million 320 hadi 520 kulingana na nafasi watakayoipata kwenye ‘kundi lao’. Hizi ni pesa zinazotengenezwa baada ya kucheza kiasi cha mechi zisizozidi 16 tu, si lelemama ndio maana kwa miaka 13 sasa timu za Tanzania zimekuwa zikiishia kucheza nane au pungufu ya hapo.
Ongezeko la Wadhamini wa Klabu
Pamoja na zawadi hizo nono zitolewazo na CAF kwa vilabu mabingwa, mafanikio ya kimataifa pia hufungua milango ya kupata wadhamini wengi zaidi. Soka ni biashara inayolipa mno hasa kwa makampuni yanayotaka kuzitangaza bidhaa na huduma zao na ulimbo pekee wa kuyanasa haya makampuni ni kwa kufika hatua za juu zaidi za michuano. Vilabu kama Al Ahly leo ina wadhamini rasmi zaidi ya tisa! (Juhayna, Shell, Egyptian Steel, Domino’s
Pizza, Coca Cola Egypt, SAIB Bank, Nestle), usiumize kichwa hata kukisia mamia ya mabilioni yanayomiminwa katika account za pale Tahrir Square, mtaa El Gabalaya jijini Cairo.
Mfano mzuri ni wakati wa mafanikio ya Simba 2003, jezi nyekundu ilichafuka kwa nembo za wadhamini. Kulikuwa na kampuni ya saruji ya pale Tegeta, benki ya makabwela Tanzania pamoja na mafuta ya kupikia ya yule bilionea kijana anayewania ridhaa ya wanachama kuimiliki klabu hiyo kwa sasa.
Mapato Yatokanayo na Viingilio U/Taifa
Watanzania huwaambii kitu kuhusiana na mapenzi yao kwenye soka. Ndio maana kila kukicha hujitokeza pale uwanja wa Taifa kutoa support kwa timu zao japo viwango wanavyo vishuhudia mara nyingi haviitendei haki pesa yao. Wastani wa million 200 mpaka 400 hukusanywa pindi timu kubwa zinapokuja kuleta ladha pale Taifa.
Iwapo timu inafanikiwa kushiriki kikamilifu hatua zote katika michuano ya kimataifa inalazimika kucheza mechi nane(8) katika uwanja wake wa nyumbani, hivyo kuna takribani billion 1.6 zinaweza kuingizwa pale Taifa ndani ya mechi nane tuu. Fikiria ile rekodi iliyowekwa May 19, 2013 katika mtanange wa Yanga vs Simba na kuingiza Tsh. 500,390,000 inavyoweza kuvunjwa mara tatu ndani ya msimu mmoja. Jumamosi anashuka Zamalek kucheza game ya marudiano fainali ya kombe la shirikisho, Jumapili wanaingia TP Mazembe ya Thom Ulimwengu kucheza game ya nusu fainali ligi ya mabingwa.
Wachezaji Binafsi Kulamba Deal za Matangazo
Kuna pengo kubwa la kimaslahi baina ya nyota wa soka bongao na wenzao wa Bongo fleva. Licha ya umaarufu wao mkubwa katika midomo ya raia mitaani lakini wanasoka wameshindwa kuvutia makampuni na taasisi zikajitangaza kupitia umashuhuri wao. Njia ya uhakika kufikia level hizo ni pindi wachezaji wenyewe watakapoamua kukunja sura mpaka watinge hatua zenye ‘heshima’. Juma Kaseja alianza kufungua hii milango wakati ule alipoenda India kushoot tangazo la kampuni ya simu ya mikononi.
Wakati umefika kwa vilabu vyote vinavyofanikiwa kupata nafasi ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya Africa kuacha kubweteka na tambo za ubingwa ambazo zimekwisha kuzoeleka katika vitongoji vya mitaa ya Kariakoo, wanachama na viongozi wanaoomba ridhaa ya kuongoza katika vilabu hivi viachane na ahadi za nipeni kura nikalipe kisasi cha vichapo vya mtani.
Huu ni muda wa kuweka malengo thabiti ya kufanya kweli Africa, huko ndipo kutawapa jeuri ya kusajili wachezaji wenye viwango vya maana na hata kuweka misingi imara ya akademi za soka. Kuna wastani wa zaidi ya Tsh. billioni 5 zinazoweza kuingizwa ndani ya msimu mmoja wa lligi, pasipo dalili ya uwepo wa wafanyakazi hewa ndani ya soka letu!
Hasta la Vista!
Instagram: @eusebius_paul

Post a Comment

 
Top