![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhfQrxVuKa6XbbtSJr2UsB5eBNf-mURIoFgbc2wMFxOYyboTUEki1poaGdgg3udA8GJTiPH8M20aKlIlvv_AUuGEHWWP0rwZbL2ZGk-_wA3qv48i-7ZEIdGdiaf-u8YHIbWRjmhPSm3gSk3/s1600/1.jpeg)
WAKURUGENZI
wawili wa Kampuni za Saha Limited na Lucky Shipping Co.Ltd,
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashitaka mawili ya uhujumu uchumi ikiwemo kupeperusha bendera ya
Tanzania bila kibali.
Washitakiwa
hao ni Issa Haji au Salum (39) ambaye ni baharia na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Lucky Shipping pamoja na Abdullah Hanga (73) mfanyabiashara
na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saha ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach.
Akisoma
mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa,
Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon alidai washitakiwa walijihusisha na
mtandao wa uhalifu kinyume na aya 4(1) C, jedwali la kwanza na kifungu
cha 57(1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu uchumi.
Saimon
alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu jijini Dar es
Salaam, walitoa ushauri, msaada na maelekezo katika kutenda kosa la
jinai la mtandao wa uhalifu ambalo ni kupeperusha bendera ya Tanzania
kwenye meli iitwayo Huihang 68 zamani ilijulikana kama Greko 02, bila
kuwa na hati ya usajili kutoka kwa msajili wa meli nchini kwa lengo la
kujipatia faida kutoka katika shughuli za uvuvi haramu.
Pia
alidai kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu, katika jiji
la Dar es Salaam washitakiwa hao huku wakifahamu kuwa ni kosa kisheria
waliruhusu upeperushwaji wa bendera katika meli hiyo ya Huihang 68 au
zamani ilijulikana kama Greko 02 bila kuwa na leseni kutoka kwa msajili
wa meli kwa lengo la kuifanya ionekane kuwa ya Tanzania wakati sio
kweli.
Hakimu Nongwa alisema washitakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Hata
hivyo, Saimon alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za
mwisho kukamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuieleza
mahakama taarifa za upelelezi huo.
Wakili
wa utetezi, Dismas Raphael aliiomba mahakama ijielekeze katika Katiba
ambayo inawatambua washitakiwa hao kama watuhumiwa na kwamba iwatendee
haki kwa kuwapatia dhamana.
Akijibu
hoja hiyo, Saimon alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP),
amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa hao kwani wakipewa
dhamana wataingilia maslahi ya Taifa hivyo mahakama ijielekeze katika
suala hilo.
Pia
alidai Ibara ya 59 (B) ibara ndogo ya 3 inaainisha mamlaka ya DPP
kuhusu masuala yote yanayolenga maslahi ya Taifa kama ilivyoainishwa
kwenye Katiba.
“Kama
upande wa utetezi wanalenga kuipinga hati ya kuzuia dhamana wanatakiwa
wafuate taratibu nyingine katika mahakama za Kikatiba ambapo
watakapowasilisha maombi yao, sisi tutayajibu ndipo mahakama itatoa
maamuzi,” alidai Saimon.
Hakimu
Nongwa alisema upande wa utetezi uwasilishe mapingamizi yao kuhusu hati
hiyo na upande wa mashitaka ujibu na kwamba mahakama hiyo itatoa
maamuzi kama hati hiyo ni sahihi au la.
Hata
hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, mwaka huu kwa ajili ya
kutajwa na kwamba washitakiwa hao wamerudishwa rumande.
Mwisho
Post a Comment