0

 Mazoezi-Yanga 5











Miamba ya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki APR na Yanga inakutana kesho Jumamosi kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika ikiwa imeshapita takribani miaka 20 tangu timu hizo zilipokutana kwenye michuano hiyo hatua ileile ya raundi ya kwanza.
APR na Yanga zinashabihiana karibu kwa kila kitu nje ya uwanja kwa siku za hivi karibuni timu hizo zikiwa zinafanya vizuri kwenye ligi zao na kutoa upinzani mkali kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi za nchi zao.
Nafasi za APR na Yanga kwenye ligi zao
APR
APR ipo nafasi ya pili kwenye ligi ya Rwanda ikiwa na pointi 30 baada ya kushuka dimbani mara 13 ikizidiwa pointi mbili na Mukura inayoongoza ligi kwa pointi 32 baada ya kucheza michezo 15 ya ligi hiyo.
Wakali hao wa Rwanda wameshinda mechi zao tano (5) zilipita huku wakishinda kwa bao 2-1 mchezo wa mwisho kwenye ligi dhidi ya Amagaju. AS Kigali wanaikimbiza APR kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi zao 28 baada ya kucheza michezo 13 wakati wapinzani wakuu wa APR timu ya Rayon Sports ikiwa imezidiwa kwa pointi nne dhidi ya wapinzani wao huku klabu hizo zikiwa zimecheza michezo sawa.
Ligi ya Rwanda ni kama ya Bongo kwa maana ya idadi ya timu ambazo zinashiriki ligi hiyo (timu 16) kwenye msimu huu wa 2015-2016.
APR imefanikiwa kufunga jumla ya mabao 18 ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mara 5 inashika nafasi ya pili kwa kuwa na magoli mengi nyuma ya Mukura yenye magoli 22 lakini yenyewe ikiwa imetunguliwa magoli 10 hadi sasa.
Yanga
Wakati APR ikiwa nafasi ya pili, Yanga yenyewe pia iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza michezo 21 huku ikiwa imezidiwa pointi moja na mahasimu wao Simba lakini Yanga inafaida ya mchezo mmoja mkononi.
Yanga inaongoza kwa kuwa timu yenye magoli mengi kwenye ligi ya Vodacom Tanzania bara ikiwa imeshafunga magoli 51 hadi sasa huku ikiwa ndiyo timu iliyofungwa magoli machache zaidi kwenye ligi (magoli 11).
Historia na mafanikio ya APR michuano ya Afrika
Klabu hiyo ambayo imeanzishwa mwaka 1993 inakutana na mabingwa wa Tanzania bara Jumamosi March 12, 2016 kwenye mechi ya raundi ya kwanza mchezo wa awali kuwania kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu. Yanga inahistoria kubwa ki-umri na mafanikio ya soka la Afrika ukilinganisha na APR ambayo bado ina umri mdogo.
Tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2012 APR imekuwa ikitolewa kati ya raundi ya awali, hadi raundi ya tatu ya CAF Champions League.
APR si klabu ya kuibeza kwasababu inamafaniko kwenye soka la ndani ya Rwanda licha ya kuanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 90 lakini tayari imeshatwaa mataji 14 ya ligi ya Rwanda kuanzia mwaka 1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009, 2010, 2011, 2012, 2014 na 2015. Pia ni bingwa mara tatu wa michuano ya CECAFA mwaka 2004, 2007 na 2010.
Wachezaji wa kigeni vs wazawa
Yanga itatumia wachezaji wake wazawa pamoja na wale wa kigeni lakini kwa upande wa APR wao walifuta sera ya kununua wachezaji wa kigeni na kuamua kutumia vijana ambao wanawaandaa wenyewe na kuwakuza na hatimaye kuwatumia kwenye kikosi chao kikosi chao kina mchezaji mmoja tu kutoka nje ya Rwanda ambaye ni straiker  Farouq Saifi Ssentongo raia wa Uganda.
Niyonzima anarejea nyumbani
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Rwanda anarejea kwenye timu yake ya zamani ambayo ilimuuza kwenda Yanga mwaka mwaka 2011.
Nyota huyo wa zamani wa APR ambaye aliichezea klabu hiyo tangu mwaka 2007-2011 amepata mapokezi ya kishujaa baada ya kukanyaga ardhi ya Rwanda.
Michuano ya CAF Champions League 2015/2016 (APR VS Yanga)
APR imeindosha klabu ya Mbabane Swallows kwa jumla ya magoli 4-2 kwenye hatua ya awali, APR ilipoteza mchezon wake wa kwanza ugenini dhidi ya  Mbabane Swallows  (February 14, 2016 Mbabane Swallows 1-0 APR) kisha ikashinda mchezo wake wa marudiano ikiwa nyumbani  (February 27, 2016 APR 4-1 Mbabane Swallows) na kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza.
Yanga yenyewe imefika raundi ya kwanza kufuatia kuitupa nje timu ya Cercle de Joachim kwa jumla ya magoli 3-0. Yanga ilianza kupata ushindi wa ugenini (February 13, 2016 Cercle de Joachim 0-1 Yanga) kisha ikaifunga tena klabu hiyo kwenye mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam  (February 202016 Yanga 2-0 Cercle de Joachim).
APR VS YANGA (HEAD TO HEAD)
Timu hizi zilikutana kwenye michuano kama hii mwaka 1996 na kushuhudia Yanga ikiaga mashindano kwa jumla ya magoli 4-1. Yanga ilianzia ugenini kama ilivyo mwaka huu, mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kuchapwa kwa bao 1-0 kabla ya kusukumwa nje ya ulingo wa CCL kwa kutandikwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa marudiano.
Tangu mwaka huo ni mwaka wa 20 sasa timu hizi hazijakutana kwenye michuano ya shirikisho la soka barani Afrika, tarajia kushuhudia mchezo mgumu uliojaa mbinu na ufundi kutokana na timu zote kuwa na rekodi nzuri kwenye ligi zao kwa sasa pamoja na michuano ya Afrika ngazi ya awali msimu huu.

Post a Comment

 
Top