
Na Baraka Mbolembole
Wawakilishi wa Tanzania bara katika michuano ya klabu bingwa Afrika, timu ya Yanga SC siku ya kesho Jumamosi watakuwa wakiwania kufuzu kwa raundi ya pili ya michuano hiyo mbele ya APR ya Kigali nchini Rwanda
Yanga iliwatoa Circle de Joachim ya Mauritius katika raundi ya awali, wakati APR iliwaondoa Mbabane Swallows ya Swaziland. Yanga wamekuwa na matokeo mazuri katika ligi ya ndani (VPL) lakini ili kuendelea kusonga mbele katika ligi ya mabingwa watapaswa kufanya jitihada kubwa, kupunguza makosa, kuongeza umakini na kuwa wastahimilivu.
Kiuchezaji kuna tatizo katika kikosi cha Yanga, kama timu kubwa hawapaswi kuingia katika mechi kwa lengo la kuzuia ndani ya dakika 15 za mwanzo na badala yake wanapaswa kucheza kwa tahadhari na kujaribu kushambulia ili wapate goli la kuongoza na si kusubiri kushambuliwa katika goli lao kwani wakifungwa mapema si nzuri kwao.
Yanga wamekuwa na mchezo wa hatari na kama wataendelea nao katika mchezo wa klabu bingwa ugenini dhidi ya APR ya Rwanda mwishoni mwa wiki hii watachapwa na kujiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele katika michuano hiyo waliyopania kufika walau hatua ya makundi (nane bora.)
YANGA DHIDI YA SIMBA SC, AZAM FC
JKT Mlale, timu ya daraja la kwanza ilitangulia kufunga wakati walipocheza na Yanga katika hatua ya 16 bora ya michuano ya FA Cup. Yanga ilikuwa na nahodha wake, Nadir Haroub na patna wake Kelvin Yondani katika beki ya kati, pia walikuwa na Mbuyu Twite na Oscar Joshua katika ngome yao ya ulinzi lakini wakakubali kutanguliwa kufungwa.
Ilikuwa ni siku chache baada ya kikosi cha Hans Van der Pluijm kuzidiwa sana katika dakika 20 za kwanza katika mechi dhidi ya mahasimu wao wa soka nchini Simba SC. Kama hiyo haitoshi, mwishoni mwa wiki iliyopita walikubali kupokea mashambulizi mengi na kurudishwa katika lango lao walipocheza na Azam FC.
Ndiyo, walitoka nyuma na kuifunga Mlale 2-1, pia wakajikusanya pamoja na kuichapa Simba 2-0, kisha wakasawazisha na kufunga goli la uongozi katika sare ya 2-2 dhidi ya Azam FC, matokeo yao yanaonesha namna walivyo na uwezo wa kufunga hata katika michezo migumu kutokana na makali ya washambuliaji wake.
Lakini kama wataendelea kucheza nyuma na kukaribisha mashambulizi katika dakika 15 za kwanza dhidi ya APR kwa kuamini wanaweza kupata matokeo kadri mechi itakavyokuwa inaendelea, halitakuwa jambo zuri.
Makocha wengi wanapenda kutoa maelekezo ya kushambulia na kuhakikisha wanapata goli la kuongoza na kulinda vizuri goli lao ndani ya dakika 15 za mwanzo. Yanga ni timu kubwa hivyo nao wanapaswa kujipanga kushambulia na kuzuia kwa uhakika mwanzoni mwa mchezo na si kucheza kwa kujihami kama ilivyokuwa dhidi ya Simba na Azam.
Uchezaji huo ni mzuri kama beki ina kuwa na uwezo wa kustahimili mashambulizi, kutopoteza umakini, lakini huwa ni hatari kwa timu kama watafungwa goli na kukutana na wapinzani makini katika kujilinda. Hans anapaswa kubadili mbinu zake wakati mwingine, hili la kuzuia mwanzoni mwa mchezo mara nyingi hufanywa na timu ndogo dhidi ya kubwa.
Yanga wanapaswa kuanza mechi kwa kushambulia si kwa kushambuliwa kama ilivyoonesha katika gemu dhidi ya Simba na Azam. Wachezaji wengi wa Yanga wamekuwa wakianza mechi taratibu na kadri dakika zinavyokuwa zinasogea nao wamekuwa wakipandisha kasi, ni nzuri ila mbaya zaidi kama utafungwa goli 2 au 3 ndani ya dakika 20.
Kitu ambacho sikipendi katika uchezaji wa Yanga ni kukubali kushambuliwa mwanzoni mwa mchezo wakati ni timu kubwa inayopaswa kuanza mechi kwa kushambulia. Yanga SC inapaswa kushambulia na si kushambuliwa.
Post a Comment