
Imefikia hatua sasa hadi Waziri Mkuu wa nchi, Mh. Kassim Majaliwa kuhoji hadharani kwanini TFF imempa tena kazi ya ukufunzi, Mdenmark, Kim Poulren wakati alionekana hafai! Kiukweli hata mimi nimeshindwa kuelewa, nashindwa kujua ni wapi Rais wa TFF, Jamal Malinzi anataka kuupeleka mpira wa Tanzania na kama atashindwa katika malengo anayokusudia ni wapi mpira wa miguu Tanzania utakapokuwa.
Miaka 8 ya utawala wa Tenga ilikuwa mibaya kwa mpira wa Tanzania. Lakini angalau aliweza kuishawishi serikali kusaidia uhamasishaji wa kusaidia makampuni, taasisi zinaingia na kusaidia udhamini kwa TFF na klabu.
Tenga alisaidia sana kuifanya TFF kuwa taasisi inayoweza kujidhamini lakini ni yeye ambaye aliumaliza mfumo wa mpira nchini kwa kuzifuta ligi za madaraja-Ligi daraja la nne, daraja la tatu, daraja la pili na ligi daraja la kwanza na kuanzisha ‘Ligi’ ambayo sijui niitaje-Ligi ya TFF ambayo ilikuwa ikitoa timu 3 za kupanda ligi kuu.
Ligi hiyo ilichezwa kati ya mwaka 2006 hadi mwishoni mwa utawala wa Tenga. Na baada ya Malinzi kuingia madarakani mwanzoni mwa mwaka 2014 alisema atarudisha mfumo wa zamani wa mpira wa miguu na kurejesha michuano mbalimbali kama Kombe la FA (tayari lipo katika msimu wake wa kwanza hivi sasa, michuano hii ilifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2002-Tenga hakuwahi kuandaa hata mara moja katika awamu zake mbili zilizopita).
Michuano ya kombe la Taifa-Taifa Cup (Tenga aliandaa kwa miaka mitatu tu katika miaka yake 8, Malinzi bado hajaandaa hata mara moja), michuano ya ligi ya Taifa ya Vijana na hapa Malinzi alitoa ahadi kwamba atahakikisha Tanzania inafuzu kwa michuano ya Afrika kufikia mwaka 2019.
Ni baadhi tu ya ahadi zake nzuri wakati akiomba kura za kuchaguliwa kuwa rais wa TFF kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho hilo la soka nchini. Kwa namna mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa kuelekea uchaguzi ule uliopangwa kufanyika Disemba, 2013 ni wazi Watanzania hakutaka kuona ‘mabaki ya watendaji’ waliokuwa katika nyakati za utawala wa Tenga wanarejea.
Baada ya Michael Wambura kuonekana hakidhi kanuni za uchaguzi, Jamal Malinzi kukatwa kwa sababu za kiuzoefu na kubaki Athuman Nyamlani kama mgombea pekee wa kiti cha urais, wadau wengi waliungana kumuunga mkono Malinzi, na ilifikia akapewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari, ambavyo vingi vilikuwa upande wake.
Nyamlani alionekana ‘kama mtu aliyepachikwa’ na Tenga kuficha udhaifu wake wa kiutawala, hivyo alipigwa vita sana. Huyu alikuwa makamu wa rais wa TFF wakati wa Tenga hivyo hakufaa. Malinzi kwangu halikuwa chaguo bora lakini nilikuwa tayari kumuunga mkono Wambura.
Si dhumuni langu kuelezea kuhusu matukio yaliyojitokeza wakati ule wa kumpata mrithi wa Tenga, lakini hata aliyekuwa naibu waziri mwenye dhamana ya michezo wakati ule, Mh. Amos Makalla aliingilia kati na kusema uchaguzi usifanyike hadi madai ya Malinzi kupinga kukatwa yatakaposikilizwa na kutolewa maamuzi sahihi.
Ni wazi naye alimtaka Malinzi, wadau walimtaka Malinzi, vyombo vya habari vilimtaka Malinzi, lakini maamuzi yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa TFF yalikuwa ‘kamari.’
Alimfuta kazi kocha Kim Poulsen na kumpa mkata wa miaka miwili mkufunzi Mholanzi, Martin Nooij ambaye aliwahi kuisaidia Msumbiji kufuzu kwa AFCON 2010. Uamuzi wake ulikuwa ni wa haraka na ulithibitisha kuwa ana mipango ya haraka ya kupata mafanikio.
Kim awali alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya vijana U17 na licha ya kwamba hakupata mafanikio katika matokeo ya uwanjani,Tenga aliamini kuwa kocha huyo ana weza kubeba majukumu ya Jan Poulsen katika timu ya Taifa Stars.
Kim aliweza kuwajumuhisha wachezaji wengi vijana mara baada ya kupewa majukumu ya kuifundisha Stars, pia alifuatilia maendeleo ya wachezaji wazoefu na hadi anaondolewa tayari alikuwa ametenga uwiano mzuri kiumri katika timu. Haruna Moshi ‘Boban’, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta wangecheza pamoja katika safu ya mashambulizi.
Frank Domayo, Salum Abubakary na Shaaban Nditti/Athumani Idd ‘Chuji’ katika kiungo na timu iliweza kucheza vizuri kule Ivory Coast pia ikaifunga 3-1 Morocco katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kim ndiye aliyemtengeza Kiemba na kumfanya kuwa ‘lulu’ tena. Alikuwa mwaminifu kwa vipaji vinavyojituma.
Siwezi kumlaumu sana Malinzi kwa kumuondoa KIM wakati ule alipoingia madarakani, lakini kutoka KIM, NOOIJ HADI SASA CHARLES MKWASSA pale Stars, kisha urejeo wa sasa wa KIM kama mkufunzi wa timu za taifa za vijana, kama mambo yatakwenda ‘mrama’ soka la Tanzania litakuwa ‘kuzimu,’ tutakuja kuliondoa ila tayari miaka 12 ya ‘Mpira Wenye Pesa’ itakuwa imekwisha.
Hivi wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF hawana mamlaka kikatiba kumpigia rais wao kura ya kutokuwa na imani naye? Kama inawezekana wakati ni sasa? KIM ameongeza ujuzi gani hadi amerudishwa kuwa kocha wa timu za Taifa?
Post a Comment